http://swahilivilla.blogspot.com/2014/01/mahojiano-na-faria-zam-kuhusu-msaada-wa.html

Monday, May 13, 2019

Polisi Tanzania inamshikilia baba aliyemtoa kafara mwanawe kwa shilingi milioni tano

Polisi Tanzania inamshikilia baba aliyemtoa kafara mwanawe kwa shilingi milioni tano
Polisi mkoani Mbeya nchini Tanzania, inashikilia watu wawili kwa kuhusika na mauaji ya mtoto wa miaka sita Rose Japhet, aliyeuawa kutokana na imani za kishirikina.

Kamanda wa Polisi katika mkoa wa Mbeya Ulrich Matei amesema uchunguzi wao umebaini kuwa mtoto huyo aliuawa tarehe 3 mwezi huu kwa kunyongwa na baadhi ya viungo vyake kunyofolewa.

Miongoni mwa watuhumiwa wa mauaji hayo ya kinyama ametajwa kuwa ni Japhet Nguku, baba mzazi wa mtoto huyo wa miaka 6. Inaelezwa kuwa chanzo cha mauji haya ni tamaa ya fedha, na baba wa msichana huyo alikubali kumuua mtoto wake ili kupata Shilingi Milioni tano za Tanzania.

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni akishiriki mazishi ya watoto waliochinjwa Njombe


Vyombo vya Habari nchini Tanzania vinaripoti kuwa baba huyo alikubali mtoto wake kuuawa kwa mfanyibiashara aliyetajwa kwa jina la Andrew Mwambuluma ambaye ni mmiliki wa Shule moja ya sekondari. Hayo yanajiri katika hali ambayo mwezi Februaria mwaka huu kulimezuka taharuki mkoani Njombe na Simiyu kutokana na wimbi la mauaji ya watoto walio chini ya umri wa miaka 10.

Mauaji yanayotokana na itikadi za kishirikina nchini Tanzania yamegeuka na kuwa kitu cha kawaida ambapo katika miaka ya hivi karibuni kumeshuhudiwa mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi, (albino) na vipara.

Serikali ya Tanzania imekuwa ikikemea visa kama hivi vya ukiukwaji wa haki za binadamu, huku wafanyabiasha na wanasiasa wakituhumiwa kuhusika ili kujipatia umaarufu na fedha kwa imani za kishirikina.

Chanzo: parstoday.com

No comments:

Post a Comment