Na Waandishi Wetu, Mwananchi
Dar/mikoani. “Reginald Mengi (75) ameondoka, Taifa limempoteza mzalendo aliyejitoa kuwasaidia wengine.” Hivi ndivyo baadhi ya watu walivyomzungumzia mwenyekiti huyo mtendaji wa kampuni za IPP.

Mengi, mfanyabiashara maarufu ndani na nje ya nchi alifariki usiku wa kuamkia jana akiwa Dubai, amegusa hisia za Watanzania wengi wakiwamo viongozi, wafanyabiashara, wanasiasa, viongozi wa dini na wasanii.
Magufuli, Kikwete
Muda mfupi baada ya taarifa za kifo kuanza kusambaa jana, Rais John Magufuli alitumia akaunti yake ya Twitter kuzungumzia kifo hicho. “Nimesikitishwa na taarifa za kifo cha Mzee na rafiki yangu Dk Reginald Mengi.”
“Nitamkumbuka kwa mchango wake mkubwa katika maendeleo ya Taifa letu na maono yake yaliyopo katika kitabu chake cha I Can, I Will, I Must. Poleni wanafamilia, wafanyakazi wa IPP na Jumuiya ya Wafanyabiashara,” aliandika Rais Magufuli
Naye Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan alitumia akaunti ya Twitter kuweka picha yake na Mengi waliyopiga pamoja kisha akaandika, “Moja ya vitu ulivyotuachia ni ule wepesi wako wa kusaidia masuala ya kijamii, daima tutakukumbuka.”
Rais mstaafu Jakaya Kikwete katika akaunti ya Twitter alindika, “Nimepokea kwa huzuni kubwa taarifa ya kifo cha ndugu yetu Dkt. Mengi. Taifa limepoteza mzalendo wa kweli na mfanyabiashara mahiri.”
“Tutamkumbuka kwa mchango wake mkubwa alioutoa kwa maendeleo ya Taifa letu na moyo wake wa upendo na huruma kusaidia jamii na hasa watu wasiojiweza.
