Na Waandishi Wetu, Mwananchi
Dar/mikoani. “Reginald Mengi (75) ameondoka, Taifa limempoteza mzalendo aliyejitoa kuwasaidia wengine.” Hivi ndivyo baadhi ya watu walivyomzungumzia mwenyekiti huyo mtendaji wa kampuni za IPP.

Mengi, mfanyabiashara maarufu ndani na nje ya nchi alifariki usiku wa kuamkia jana akiwa Dubai, amegusa hisia za Watanzania wengi wakiwamo viongozi, wafanyabiashara, wanasiasa, viongozi wa dini na wasanii.
Magufuli, Kikwete
Muda mfupi baada ya taarifa za kifo kuanza kusambaa jana, Rais John Magufuli alitumia akaunti yake ya Twitter kuzungumzia kifo hicho. “Nimesikitishwa na taarifa za kifo cha Mzee na rafiki yangu Dk Reginald Mengi.”
“Nitamkumbuka kwa mchango wake mkubwa katika maendeleo ya Taifa letu na maono yake yaliyopo katika kitabu chake cha I Can, I Will, I Must. Poleni wanafamilia, wafanyakazi wa IPP na Jumuiya ya Wafanyabiashara,” aliandika Rais Magufuli
Naye Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan alitumia akaunti ya Twitter kuweka picha yake na Mengi waliyopiga pamoja kisha akaandika, “Moja ya vitu ulivyotuachia ni ule wepesi wako wa kusaidia masuala ya kijamii, daima tutakukumbuka.”
Rais mstaafu Jakaya Kikwete katika akaunti ya Twitter alindika, “Nimepokea kwa huzuni kubwa taarifa ya kifo cha ndugu yetu Dkt. Mengi. Taifa limepoteza mzalendo wa kweli na mfanyabiashara mahiri.”
“Tutamkumbuka kwa mchango wake mkubwa alioutoa kwa maendeleo ya Taifa letu na moyo wake wa upendo na huruma kusaidia jamii na hasa watu wasiojiweza.
Kikwete aliongeza, “Natoa pole zangu nyingi kwa familia yake na wafanyakazi wote wa IPP. Tunawaombea kwa Mwenyezi awape moyo wa subra na ustahimilivu katika kipindi hiki kigumu cha majonzi na kuomboleza.”
...Wanasiasa walivyomlilia
Katika salamu zake za rambirambi, mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema itachukua miaka mingi kumpata mtu kama Mengi.
Akizungumza nyumbani kwa Mengi, Kinondoni jijini Dar es Salaam, alisema Mengi alikuwa mtu wa watu wote aliyewajali walemavu, wanamichezo pamoja na tasnia ya habari. “Kwa niaba ya wananchi wa Hai, wanachama wa vyama vyote hasa wana-Chadema pamoja na Watanzania nitoe pole kwa wote walioguswa na msiba huu,” alisema Mbowe ambaye pia ni kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni.
“Itachukua miaka mingi kumpata mtu kama Mengi, alikuwa mdau mwekezaji, alijali wanyonge, kuondoka kwake ni pigo kubwa kwa Taifa.”
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, January Makamba alisema Mengi alikuwa ni nembo ya Tanzania duniani.
Akizungumza katika viwanja vya Bunge jijini Dodoma, Makamba alisema alikuwa na mchango mkubwa katika tasnia ya habari, biashara na mazingira. “Ni nembo ya Tanzania duniani kwa sababu akitajwa katika majarida mbalimbali, pembeni mwa jina lake inatajwa Tanzania, alikuwa balozi wa Tanzania,” alisema.
Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alisema pengo la Mengi ni gumu kuzibika na daima mchango wake utaendelea kuthaminika.
Akitumia akaunti yake ya Facebook, Ummy alisema, “Pumzika kwa amani kaka (Dk Mengi).
Viongozi wa dini
Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk Fredrick Shoo alisema jana kuwa Mengi atakumbukwa kwa mchango mkubwa kwa kanisa hilo, jamii na Tanzania kwani alijitoa kwa dhati kuwasaidia watu wanyonge na maskini.
“Nimekipokea kwa masikitiko makubwa kifo cha Reginald, alijitoa sana kuwasaidia watu wanyonge. Mchango wake kwa maendeleo ya jamii na kanisa ni mkubwa sana,” alisema Askofu Shoo
“Tumeondokewa na mtu ambaye Mungu alimjalia kuutumia utajiri wake kuwasaidia wengine. Tunamshukuru Mungu kwa mema mengi tuliyoyapokea kutoka kwake.”
Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salum alisema enzi za uhai wake Mengi alijitoa kwa hali na mali kutoa misaada mbalimbali ikiwamo ujenzi wa madrasa na misikiti akitoa mfano msikiti wa Muheza mkoani Tanga.
“Alikuwa rafiki wa watu, hakubagua dini wala kabila, alikuwa mhamasishaji wa amani na mshauri pia,” alisema
Kiongozi huyo wa dini alisema Mengi ndiye mwanzilishi wa kamati ya amani ya viongozi wa dini akishirikiana na Rais mstaafu wa awamu ya pili, Ally Hassan Mwinyi.
“Lakini pia alikuwa mwepesi wa kutoa misaada, nakumbuka kuna kipindi niliomba awafungulie maimamu akaunti alifanya hivyo bila kusita.”
Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Askofu Gervas Nyaisonga alisema watamkumbuka kwa ukarimu na utayari wa kushiriki harambee mbalimbali za maendeleo ya dini.
Alisema Mengi alikuwa na ujasiri wa kukemea mambo ambayo wengi waliogopa kufanya hivyo.
“Mengi aligusa maisha ya watu wengi mbali na kuwa mtu mashuhuri, lakini hakubagua mtu, alisaidia wenye shida, aliwashika mkono walemavu naweza kusema alikuwa na mko Viongozi TPSF, CTI wazungumza ni mwepesi,” alisema Gervas ambaye pia ni askofu Katoliki Jimbo Kuu la Mbeya.
Wasanii wamtaja kuwa kioo
Wakimzungumzia Mengi, baadhi ya wasanii wamemtaja kuwa kioo cha mafanikio ya Watanzania.
Msanii Nandy kupitia ukurasa wake wa Instagram aliandika, “Pole sanaa wanafamilia pumzika kwa amani mzee Mengi.”
Mahsin Awadh maarufu Dk Cheni kupitia ukurasa wa Instagram aliandika “apumzike kwa amani, kweli kifo ni cha wote uwe na mali uwe, masikini wote tutalala sehemu moja Mungu akupe pumziko la amani. Tangulia nasi tunakufuata pole sana.”
Naseeb Abdul maarufu Diamond Platnumz, aliandika kwenye ukurasa wake wa Instagram, ni habari mbaya na anamuombea apumzike kwa amani.
Mwigizaji wa vichekesho Sylvester Mujuni maarufu Mpoki kupitia mtandao wa Instagram aliandika Mengi aliwaonyesha vijana jinsi ya kupenda na kutafuta fedha.
Naye mwimbaji Ommy Dimpoz kupitia ukurasa wake wa Instagram aliandika, “Innalilaahi Wainailaahi Raajun Tutakukumbuka kwa Mengi mazuri kama jina Lako R.I.P Chairman #IcanImustIwill”.
Chanzo: swahilihub.com

No comments:
Post a Comment