Takeshi Iwaya ametoa onyo hilo kufuatia mauaji ya mwanamke mmoja raia wa Japan aliyeuawa na askari wa Marekani katika eneo hilo na kusema kuwa, ni lazima Washington idhibiti mienendo mibaya ya askari wake katika kisiwa cha Okinawa, sambamba na kuhitimisha hali ya ukosefu wa udhibiti kati ya askari hao.
Aidha Waziri wa Ulinzi wa Japan amebainisha kwamba wakazi wa kisiwa hicho wana wasi wasi mkubwa kutokana na uwepo wa askari wa Kimarekani katika kisiwa hicho na amebainisha kwamba ili kuzuia matukio yanayotokana na utumiaji mabavu wa askari hao katika eneo hilo, kuna haja ya kuchukuliwa hatua madhubuti katika uwanja huo.
Askari wa Marekani walioko katika kisiwa cha Okinawa
Inafaa kuashiria kuwa, siku chache zilizopita askari mmoja wa Marekani mwenye umri wa miaka 32, alimuua mwanamke mmoja raia wa Japan katika kisiwa cha Okinawa kwa kumchoma kisu kisha naye akajiua.
Indhari ya Waziri wa Ulinzi kwa Marekani kuhusiana na vitendo vya ukatili wa askari wa Kimarekani dhidi ya raia wa Japan imekuja kutokana na wasi wasi mkubwa iliyonayo serikali ya Tokyo juu ya uwezekano wa kuibuka matukio yasiyotarajiwa ya wakazi wa Okinawa kuwalenga askari hao wa kigeni.
Kwa mujibu wa takwimu, askari wa Kimarekani waliopo katika kisiwa hicho cha Japan walihusika na vitendo vya ubakaji kwa zaidi ya wanawake 1000 kati ya mwaka 2005 hadi 2013.
Source: parstoday.com

No comments:
Post a Comment