Mbunge machachari wa Uganda Robert Kyagulanyi na mpinzani mkongwe Dakta Kizza Besigye wametangaza kuungana na kushirikiana katika uchaguzi ujao ili kukiondoa madarakani chama tawala cha Rais Yoweri Museveni cha National Resistance Movement (NRM).
Taarifa ya pamoja iliyotolewa na wanasiasa hao imeonyesha kwamba baada ya mashauriano kati yao wamefikia makubaliano kuhusu masuala kadhaa kwa ajili ya kushirikiana kisiasa katika uchaguzi ujao dhidi ya chama cha Rais Museveni ambacho kimekuwa madarakani nchini Uganda tangu mwaka 1986.
Akizungumza na waandishi habari Mbunge Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine alisema wamekuwa wakishauriana katika mikutano kadhaa na vyama tofuati vya kisiasa nchini Uganda kikiwemo cha Democratic Party maarufu DP na hivi karibuni na kiongozi wa People's government, Dkt Kizza Besigye.
"Tunaungana na vikosi vingine vya kutaka mageuzi, tunajua kwamba ili kuufanikiwa katika mapambano haya, kuna haja kwa sisi kuwa pamoja, amesema Bobi Wine.
Rais Yoweri Museveni wa Uganda
Bobi Wine ambaye amejizolea umashuhuri katika miezi ya hivi karibuni, alipandishwa kizimbani katika mahakama moja jijini Kampala na kusomewa mashtaka ya kuandaa mkutano na kufanya maandamano kinyume cha sheria mwaka 2018 na baadaye kuzuiwa katika Gereza la Luzira kabla ya kuachiliwa huru baadaye.
Kwa upande wake, Kizza Besigye anayehesabiwa kuwa kiongozi mkongwe wa upinzani nchini Uganda amewahi kugombea mara kadhaa kiti cha urais na kushindwa na Rais Museveni.
Wapinzani nchini Uganda wamekuwa wakilalamikia kile wanachokitaja kuuwa, "mkono wa chuma wa serikali" dhidi ya wapinzani hatua ambayo wanasema inakandamiza na kubinya demokrasia katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki.
Chanzo: parstoday.com
