Rais Donald Trump wa Marekani ameahidi kuwa iwapo atashinda muhula wa pili katika uchaguzi wa rais mwaka ujao, basi utawala wake utatoa tiba ya maradhi hatari ya saratani na Ukimwi.
Trump aliyasema hayo jana jioni katika mji wa Orlando jimboni Florida wakati akizindua kampeni za kugombea urais kwa muhula wa pili mwaka ujao 2020, ambapo amebainisha kuwa, "Tutatibu magonjwa mengi kama vile saratani na mengine mengi. Tutauondoa Ukimwi nchini kikamilifu. Tunakaribia sana kufikia jambo hilo."
Kadhalika Trump amewaahadaa Wamarekani kwa kusema kuwa, "Tutaweka msingi wa kuhakikisha wanaanga wa Marekani wanatua katika sayari ya Mirihi (Mars)."
Maandamano dhidi ya Trump mbele ya Ikulu ya White House
Trump amezindua kampeni ya kuwania muhula wa pili wa urais katika hali ambayo, siku chache zilizopita maelfu ya wananchi wa Marekani walifanya maandamano katika miji tofauti inayokaribia 130 ya Marekani wakitaka Trump asailiwe.
Aidha Trump amezindua kampeni hiyo iliyojaa porojo na hadaa wakati huu ambapo tafiti za maoni zinaonesha kuwa, rais huyo wa Marekani anaendelea kupoteza umashuhuri na imani kwa Wamarekani, akishindwa na mahasimu wake wakubwa wa kisiasa wa chama cha Democtars akiwemo Joe Biden, makamu wa rais wa zamani wa nchi hiyo.
Chanzo: parstoday.com
