http://swahilivilla.blogspot.com/2014/01/mahojiano-na-faria-zam-kuhusu-msaada-wa.html
Showing posts with label Mazungumzo kuhusu utawala wa kiraia Sudan kufanyika leo. Show all posts
Showing posts with label Mazungumzo kuhusu utawala wa kiraia Sudan kufanyika leo. Show all posts

Monday, May 13, 2019

Mazungumzo kuhusu utawala wa kiraia Sudan kufanyika leo

Mazungumzo kuhusu utawala wa kiraia Sudan kufanyika leo
Baraza la Mpito la Kijeshi la Sudan na viongozi wa maandamano nchini humo leo wanatarajiwa kuanza duru mpya ya mazungumzo kuhusiana na suala la kukabidhiwa madaraka ya nchi hiyo kwa utawala wa kiarai.

Hayo yameelezwa na wasemaji wa pande mbili hizo ambao wameeleza kwamba, mazungumzo hayo yanalenga kuupatia ufumbuzi mkwamo wa mchakato wa kukabidhiwa madaraka ya nchi hiyo kwa utawala wa kiraia. Mazungumzo hayo yalipangwa kufanyika jana Jumapili lakini yakaakhirishwa hadi leo.

Viongozi wa maandamano nchini Sudani wamekuwa wakilituhumu Baraza la Mpito la Kijeshi nchini humo kwamba, linapoteza muda na hivyo kuchelewesha mchakato wa kukabidhi madaraka kwa utawala wa kiraia.

Waandamanaji hao wanasisitiza kwamba, Baraza la Mpito la Kijeshi linapaswa kukabidhi madaraka kwa utawala wa kiraia kama lilivyoahidi.

Maandamano ya wananchi wa Sudan

Licha ya kwamba jeshi la Sudan liliahidi kukabidhi madaraka kwa utawala wa kiraia baada ya maandamano kumng'oa madarakani rais wa zamani wa nchi hiyo, Omar Hassan al Bashir, lakini hadi sasa limeshindwa kutekeleza ahadi yake hiyo.

Baraza la Mpito la Kijeshi la Sudan liliundwa baada ya mapinduzi ya kijeshi ya tarehe 11 mwezi uliopita wa Aprili, mapinduzi ambayo yalihitimisha utawala wa takriban miaka 30 wa Jenerali Omar Hassan al Bashir.

Wapinzani nchini Sudan wanasisitiza kuwa, madhali Baraza la Mpito la Kijeshi halijakabidhi madaraka ya nchi kwa utawala wa kiraia maandamano na malalamiko ya wananchi wa nchi hiyo yataendelea kushuhudiwa.

Chanzo: parstoday.com