Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres amezindua kampeni kabambe ya kuhimiza hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi, yanayoelezewa kuwa suala muhimu kabisa kwa wakati huu kuhusu mustakabali wa dunia.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres (kushoto) na Waziri Mkuu wa New Zealand, Jacinda Ardern mjini Auckland
Ziara hiyo ya Katibu Mkuu Guterres iliyoanzia New Zealand itamfikisha pia katika visiwa vingine kadhaa vya Kusini mwa Bahari ya Pasifiki, vikiwemo Fiji, Tuvalu na Vanuatu, ambavyo vimetajwa kuwa kwenye mstari wa mbele katika kukabiliwa na athari zitokanazo na mabadiliko ya tabianchi. Kupanda kwa kina cha bahari kunakokwenda sambamba na kuongezeka kwa joto duniani kunatishia kuvizamisha visiwa hivyo na kuyaweka hatarini maisha ya wakazi wake.
Akizungumza na waandishi wa habari pamoja na waziri mkuu wa New Zealand Jacinda Ardern, Guterres ameisifu New Zealand kwa sera zake rafiki kwa mazingira, akaonya lakini kwamba ari ya kisiasa kushughulikia mabadiliko ya hali ya hewa, imekuwa ikipungua. Katibu Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa amewatolea mwito vijana kuongoza mipango ya kuyalinda mazingira ya dunia, akisema nchi zilizo na viongozi wenye umri mdogo zimekuwa zikiongoza utekelezwaji wa sera za kuzuia uchafuzi wa mazingira ya dunia.
Apinga matumizi ya kodi kwa ruzuku ya nishati chafu
Kwa hali ya kipekee, Guterres amezitaka serikali za nchi kuacha kutumia fedha za walipa kodi kudhamini shughuli za kiuchumi ambazo zinalaumiwa kuiweka dunia katika hatari iliyopo.
Wakazi wa visiwa vidogo wanatishiwa na kina cha bahari kinachozidi kupanda
''Ni ujumbe ulio wazi kwa serikali, kwamba ni muhimu kabisa kuacha kutumia fedha za walipa-kodi kutoa ruzuku kwa matumizi ya nishati chafu. Hilo ni kutumia pesa za walipa-kodi kuongeza vimbunga, kueneza ukame, mawimbi ya joto kali, kuangamiza matumbawe na kuharakisha kuyeyuka kwa theluji.'' Amesema Guterres na kuongeza kwamba fedha za walipa-kodi zinapaswa kuwekezwa katika maeneo yenye manufaa kwa ubinadamu.
