Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Cuba amekanusha tuhuma na kupuuza vitisho vya hivi karibuni vya Marekani dhidi ya nchi yake na kusisitiza kwamba, Havana haina vikosi vya kijeshi huko nchini Venezuela.
Bruno Rodriguez amesema hayo katika radiamali yake kwa matamshi ya hivi karibuni ya John Bolton Mshauri wa Usalama wa Taifa wa Ikulu ya Marekani White House na kusema wazi kwamba, Bolton anaugua maradhi ya kusema uongo na kwamba, amekuwa akimpatia Rais Donald Trump taarifa za uongo kabisa.
Akijibu tuhuma za serikali ya Marekani dhidi ya nchi yake, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Cuba ameandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter kwamba: Havana haijatuma wanajeshi huko Venezela kama inavyodaiwa Washington na si kweli kwamba, nchi yetu imekuwa ikivuruga amani na usalama katika nchi hiyo.
John Bolton, Mshauri wa Usalama wa Taifa wa Rais Donald Trump wa Marekani
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Cuba amesisitiza kuwa, John Bolton anaugua maradhi ya kusema uongo na amekuwa akimpotosha Rais Donald Trump.
Ameongeza kuwa, Cuba haina nafasi yoyote ile katika operesheni ya kijeshi na kiusalama ya Venezuela na ilichokifanya serikali ya Havana ni kutuma timu za madaktari na wahudumu wa sekta ya afya ambao wako nchini humo kutekeleza majukumu yao katika uga wa masuala ya kibinadamu.
Rais Donald Trump alinukuliwa hivi karibuni akitishia kwamba, atafanya mapinduzi ya kijeshi nchini Cuba na kuiwekea Havana vikwazo vikali kabisa endapo nchi hiyo haitaondoa vikosi vyake vya kijeshi huko Venezuela, vitisho ambayo vimepuuzwa na viongozi wa nchi hiyo.
Chanzo: hparstoday.com
