Waziri wa Mambo ya Ndani wa Kenya Kipchumba Murkomen, amesema jukumu la kudhamini usalama linalotekelezwa na kikosi cha usaidizi cha mataifa kadhaa (MSS) kikiongozwa na nchi hiyo huko Haiti linazidi kuimarishwa na kupata nguvu zaidi ikiwa ni uthibitisho wa namna taifa hilo la mashariki ya Afrika linavyotimiza ahadi yake kwa Jamii ya Kimataifa.
Murkomen ametoa kauli hiyo sambamba na taarifa yake katika mtandao wa X kwamba, Kenya imetuma askari wengine 144 nchini Haiti, kujaribu kulinda amani na kurejesha utulivu nchini humo.
Askari hao, ambao ni wa kiume 120 na wa kike 24, wameelekea Haiti asubuhi ya Alkhamisi Februari 6, 2025 baada ya kuagwa na waziri huyo wa mambo ya ndani wa Kenya.
Idadi hiyo inafikisha jumla ya askari polisi 744 wa Kenya waliotumwa nchini Haiti kwa ajili ya kupambana na magenge ya kihalifu yaliyokithiri nchini humo.
“Leo nimewaaga askari wengine 144 ili kuweza kuongeza nguvu kwa wenzao waliotangulia, na tayari tunaona maendeleo mazuri huko Haiti,” aliandika Murkomen katika ukurasa wake wa X.
Mbali na Kenya, nchi zingine, zikiwemo Guatemala na El Salvador zimeongeza idadi ya askari wao ziliowapeleka huko Haiti ili kujaribu kudhibiti magenge ya wahalifu.
“Tunaendelea kuwasiliana Umoja wa Mataifa pamoja na nchi zinazounga mkono hatua ya kutuliza ghasia nchini Haiti, ikiwemo Marekani,” ameongezea kueleza Murkomen.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya ameeleza hayo sambamba na nchi hiyo kutangaza hivi majuzi kuwa imeanzisha mchakato wa kubadilisha ujumbe wake wa usalama ulioko Haiti kuwa operesheni ya Umoja wa Mataifa, baada ya Marekani kusimamisha ufadhili wake wa kifedha kwa ujumbe huo.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Kenya, Korir Sing’oei amesema, licha ya Marekani kuzuia ufadhili huo kwa muda wa siku 90, ujumbe huo wa kurejesha usalama na utulivu nchini Haiti utaendelea kufanya kazi kwa kutumia rasilimali zilizopo.../
CHANZO: https://parstoday.ir/sw/news/africa

No comments:
Post a Comment