Mamia ya wananchi wa Jamhuri ya Afrika ya Kati wameandamana kupnga mpango wa kufanyia marekebisho katiba ya nchi na kuidhinisha muhula wa tatu kwa Rais.
Viongozi wa upinzani katika Jamhuri ya Afrika ya Kati wameongoza maandamano katika mji mkuu Bangui yaliyosindikizwa na vikosi vya usalama vya CAR na magari ya ujumbe wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa MINUSCA.
Mamia ya watu walijitokeza katika maandamano hayo na kupuuza marufuku ya maandamano ya kupinga mipango ya mabadiliko ya katiba ambayo yatamuwezesha rais wa Jamhuri ya Afrika ya Kati kuwania uchaguzi kwa muhula wa tatu.
Zoezi la upigaji kura linatarajiwa kufanyika Julai 30 kwa ajili ya mabadiliko yanayopendekezwa kwenye katiba ya Jamhuri ya Afrika ya Kati.
Iwapo itaidhinishwa, itamaanisha kuwa mihula miwili iliyowekwa na katiba itafutwa na hivyo kumuwezesha Rais Faustin Archange Touadera kuwania muhula mwingine madarakani, kulingana na wafuasi wake.
Touadera alichaguliwa tena mwaka 2021 katika uchaguzi uliolalamikiwa na ambayo ulikosolewa vikali kwa idadi ndogo ya wapiga hasa kwa sababu ya vitisho katika maeneo yanayodhibitiwa na waasi.
Machafuko huko Jamhuri ya Afrika ya Kati yalizuka mwaka 2013, baada ya waasi wa Seleka kumuondoa madarakani aliyekuwa rais wa nchi hiyo, François Bozizé.
Baada ya Rais Michel Djotodia kuchukua mamlaka, waasi wa Kikristo wenye misimamo ya kufurutu ada wa Anti-Balaka walianzisha mauaji ya kimbari dhidi ya jamii ya Waislamu, ambapo maelfu ya Waislamu waliuawa na wengine wengi kulazimika kuwa wakimbizi.

No comments:
Post a Comment