http://swahilivilla.blogspot.com/2014/01/mahojiano-na-faria-zam-kuhusu-msaada-wa.html

Sunday, July 7, 2019

Baraza la Kijeshi Sudan: Tutatekeleza makubaliano yetu na wapinzani

Baraza la Kijeshi Sudan: Tutatekeleza makubaliano yetu na wapinzani
Mkuu wa Baraza la Kijeshi la Mpito la Sudan ameahidi kwamba, baraza hilo litatekeleza kikamilifu makubaliano yaliyofikiwa kati yake na Muungano wa Uhuru na Mageuzi na kwamba, linaunga mkono makubaliano hayo.

Abdul Fattah al Burhan amesema hayo katika hotuba yake kwa umma iliyorushwa mubashara na televisheni ya taifa na kueleza kwamba, kutiwa saini makubaliano kati ya baraza hilo la kijeshi la mpito na muungano wa vyama vya upinzani kumepelekea taa ya mapinduzi kuwaka zaidi.

Mkuu wa Baraza la Kijeshi la Mpito la Sudan amesema kuwa, kwa sasa tumo katika hatua ya kuanzisha Sudan mpya ambayo watu wote watashirikishwa na ndani yake kutaheshimiwa haki za raia na wakati huo huo kutaendeshwa vita dhidi ya ufisadi.

Ameongeza kuwa, Baraza la Kijeshi la Mpito la Sudan litafanya kila liwezalo ili kuhakikisha kwamba, amani, uhuru na uadilifu vinashuhudiwa nchini Sudan.

Moja ya vikao vya mazungumzo kati ya Baraza la Kijeshi la Mpito na viongozi wa Muungano wa Uhuru na Mageuzi nchini Sudan

Hivi karibuni Baraza la Kijeshi la Mpito nchini Sudan na muungano wa upinzani wa Uhuru na Mageuzi waliafikiana juu ya suala la kugawana madaraka katika kipindi cha mpito cha miaka mitatu kuelekea katika uchaguzi mkuu.

Baraza la Kijeshi la Sudan lilichukua madaraka tarehe 11 Aprili mwaka huu baada ya jeshi la nchi hiyo kumpindua Omar Hassan al-Bashir aliyyekuwa raia wa nchi hiyo.

Tangu wakati huo Sudan iliendelea kushuhudia maandamano ya wananchi ya kulishinikiza Baraza la Kijeshi la Mpito likabidhi madaraka ya nchi kwa utawala wa kiraia.

Source: parstoday.com

No comments:

Post a Comment