http://swahilivilla.blogspot.com/2014/01/mahojiano-na-faria-zam-kuhusu-msaada-wa.html

Thursday, June 6, 2019

Russia na China zalaani vikwazo vya upande mmoja vya Marekani dhidi ya Iran

Russia na China zalaani vikwazo vya upande mmoja vya Marekani dhidi ya Iran
Marais wa Russia na China sanjari na kulaani vikwazo vya upande mmoja vya Marekani dhidi ya Iran, lakini pia wamezitaka pande husika kufungamana na makubaliano ya nyuklia ya Vienna yanayojulikana kama JCPOA.

Marais Vladimir Putin na Xi Jinping wamesema hayo katika taarifa ya pamoja mjini Moscow na kubainisha kuwa, pande zilizosalia kwenye mapatano hayo ya kimataifa zina wajibu wa kuendelea kufungamana na kuheshimu makubaliano hayo.

Wawili hao wamesema wameridhishwa na ripoti za Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA zilizothibitisha kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imefungamana na kutekeleza wajibu wake kwenye makubaliano hayo.

Kadhalika marais wa Russia na China wamekosoa vikali sera haribifu ya Marekani ya vikwazo vya upande mmoja dhidi ya Iran, wakisisitiza kuwa nchi zao zitaendelea kufungamana na makubaliano ya JCPOA kwa mujibu wa Azimio Nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na Sura ya 25 ya Mkataba wa UN.

Marais wa Russia na China mjini Moscow

Hali kadhalika wameitaka Iran isichukue hatua yoyote zaidi ya kutofungana na JCPOA. Hivi karibuni, Rais Hassan Rouhani alitangaza kuwa Iran imesitisha utekelezaji wa baadhi ya vipengee vya JCPOA, na kuupa Umoja wa Ulaya siku 60 utekeleze ahadi zake zinazohusiana na makubaliano hayo, vinginevyo itachukua hatua zaidi.


Hapo jana Rais wa China muda mfupi kabla ya kuonana na mwenyeji wake Vladimir Putin wa Russia aliwaambia waandishi wa habari kuwa, mashinikizo ya kiwango cha juu na vikwazo vya upande mmoja vya Marekani dhidi ya Iran ndiyo chimbuko la kushtadi taharuki katika eneo la Asia Magharibi.

Marais wa Russia na China wamesisitiza kuwa nchi zao zitaendelea kuimarisha na kukuza katika kiwango cha juu zaidi uhusiano wa pande mbili katika nyuga mbalimbali.

Chanzo: parstoday.com

No comments:

Post a Comment