Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Mauritania imetangaza rasmi kuwa, waziri wa zamani wa ulinzi wa nchi hiyo, Mohammad Ould Ghazouani ndiye mshindi katika uchaguzi wa rais wa hivi karibuni nchini humo. Ghazouani ni mtu wa karibu sana na rais wa hivi sasa wa nchi hiyo, Mohammed Ould Abdel Aziz.
Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Mauritania imesema kuwa, Ghazouani ameshinda uchaguzi huo kwa kupata asilimia 52.01 ya kura.
Mkuu wa tume hiyo ya uchaguzi, Ould Bilal, amewaambia waandishi wa habari kwamba uchaguzi huo ni ushindi kwa taifa la Mauritania na umetia nguvu misingi ya kidemokrasia nchini humo.
Amedai kuwa tume yake imeendesha uchaguzi huo kwa uwazi na kwa usalama kabisa. Mashirika ya habari yanasema kuwa asilimia 66.62 ya watu waliotimiza masharti ya kupiga kura wameshiriki kwenye uchaguzi huo.
Kampeni za uchaguzi nchini Mauritania
Jana Jumapili mgombea huyo urais wa chama tawala nchini Mauritania alijitangaza mshindi katika uchaguzi huo wa siku ya Jumamosi ya tarehe 22 Juni, 2019 kabla ya kutolewa matokeo rasmi.
Wakati mgombea huyo akijitangaza mshindi, wagombea wa upinzani, Sidi Mohamed Ould Boubacar, waziri mkuu wa zamani, na Biram Ould Dah Ould Abeid walikuwa wamepata asilimia 18 tu ya kura kila mmoja wakati zoezi la kuhesabu kura likiendelea.
Wagombea hao wa upinzani wamelalamikia dosari zilizokuwepo katika zoezi la kupiga kura na kudai kwamba wawakilishi wao walitimuliwa kutoka baadhi ya vituo vya kupigia kura. Hata hivyo Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Mauritania CENI imesema hakuna matatizo makubwa yaliyoripotiwa katika upigaji kura huo.
Chanzo: parstoday.com

No comments:
Post a Comment