Wizara ya Mambo ya Nje ya Korea Kaskazini imetoa taarifa yenye kuionya serikali ya Marekani ikiitaka ihitimishe hatua zake hasi dhidi ya nchi hiyo.
Katika taarifa hiyo iliyotolewa jana jioni, Wizara hiyo ya Mashauri ya Kigeni ya Korea Kaskazini imeitahadharisha Washington kwamba ni lazima ibadili siasa zake hizo na kwamba kinyume na hivyo, isubiri jibu kali kutoka Pyongyang.
Aidha imesema kuwa, iwapo Marekani itaendeleza mashinikizo yake yasiyovumilika dhidi ya serikali ya Pyongyang kwa ajili ya kuitaka nchi hiyo itokomeze silaha zake za nyuklia, basi itakuwa imehatarisha taarifa iliyotolewa mwishoni mwa kikao cha viongozi wa nchi mbili nchini Singapore ambayo iliitaka nchi hiyo kuangamiza silaha zake za nyuklia katika Rasi ya Korea na pia kudhaminiwa usalama wake.
Mazungumzo ya viongozi wa nchi mbili
Itakumbukwa kuwa Kim Jong-un wa Korea Kaskazini na Rais Donald Trump wa Marekani walikutana tarehe 12 Juni mwaka jana nchini Singapore ambapo walitiliana saini makubaliano hayo. Hata hivyo baada ya duru ya mazungumzo ya viongozi hao hao kuvunjika huko mjini Hanoi, Vietnam mwezi Februari mwaka huu, mazungumzo hayo yamekwama hadi sasa. Kupenda makubwa kwa Trump kunatajwa kuwa sababu kuu ya kuvunjika mazungumzo hayo.
Chanzo: parstoday.com

No comments:
Post a Comment