http://swahilivilla.blogspot.com/2014/01/mahojiano-na-faria-zam-kuhusu-msaada-wa.html

Saturday, June 8, 2019

Kikao cha Rais Magufuli Tanzania, chaondoka na Waziri wa Viwanda na Kamishna wa TRA

Kufuatia kikao cha jana cha Rais John Pombe Magufuli wa Tanzania na wafanyabiashara kutoka wilaya zote za nchi hiyo, kiongozi huyo amempiga kalamu nyekundu Joseph Kakunda, Waziri wa Viwanda na Biashara na kumteua mahala pake Innocent Bashungwa kuongoza wizara hiyo.

Viongozi wapya walioteuliwa na Rais Magufuli katika mabadiliko madogo, ya Wizara ya Viwanda na TRA
Viongozi wapya walioteuliwa na Rais Magufuli katika mabadiliko madogo, ya Wizara ya Viwanda na TRA

Innocent Bashungwa alikuwa Naibu Waziri wa Kilimo ambapo sasa ataongoza Wizara ya Viwanda na Biashara. Aidha Rais Magufuli amemteua Edwin Mhede kuwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), ambaye amechukua nafasi ya Charles Kichere aliyekuwa akiongoza mamlaka hiyo muhimu ya kukusanya mapato. 

Taarifa iliyotolewa leo na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Gerson Msigwa imesema kuwa Rais amemteua Charles Kichere, aliyekuwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Njombe akichukua nafasi ya Erick Shitindi ambaye amestaafu. 

Kamishna Mkuu mpya wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Edwin Mhede kabla ya uteuzi huu, alikuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara. Kufuatia mabadiliko hayo, aliyekuwa Waziri wa Viwanda na Biashara, Joseph Kakunda amesema kuwa alitaraji Rais John Magufuli kumuondoa katika wizara hiyo.

Rais John Pombe Magufuli wa Tanzania

Kwa mujibu wa Kakunda, alilitarajia hilo kutokana na mazingira yaliyokuwepo jana kwenye mkutano kati ya Rais John Magufuli na wawakilishi wa wafanyabiashara kutoka wilaya zote nchini Tanzania uliofanyika Ikulu, Dar es Salaam.


Kakunda amepigwa kalamu nyekundu akiwa ametimiza siku 210 tangu alipoteuliwa kuongoza Wizara hiyo ambapo alichukua mikoba kutoka kwa Charles Mwijage ambaye pia aliondolewa na rais akiwa na muda mchache katika wizara hiyo. 

Amebainisha kwamba, namna wafanyabiashara walivyotoa malalamiko yao ikulu na kuinyooshea kidole Wizara ya Viwanda wakidai haiwatendei haki, alibaini kukumbwa na panga hilo la Rais Magufuli au kwamba angelazimika kujiuzulu. Katika kikao hicho cha jana Rais Magufuli alisema kuwa anatamani wakati atakapomaliza muda wake wa uongozi, Tanzania iwe na mabilionea zaidi ya 100.

Source: parstoday.com

No comments:

Post a Comment