http://swahilivilla.blogspot.com/2014/01/mahojiano-na-faria-zam-kuhusu-msaada-wa.html

Thursday, June 20, 2019

Erdogan: Morsi ameuliwa; serikali ya Misri inapasa kuchukuliwa hatua

Erdogan: Morsi ameuliwa; serikali ya Misri inapasa kuchukuliwa hatua
Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki ametaka kufunguliwa mashtaka maafisa wa serikali ya Misri waliomuua Mohamed Morsi, Rais wa kwanza wa nchi hiyo kuchaguliwa kidemokrasia.

Akizungumza jana katika kampeni za uchaguzi, Rais wa Uturuki amebainisha kuwa Morsi hakufa hivi hivi tu bali aliuliwa. Itakumbukwa kuwa Mohamed Morsi aliaga dunia Jumatatu wiki hii akiwa mahakamani huko Cairo wakati kesi iliyokuwa ikimkabili ikisikilizwa. 

Erdogan ameongeza kuwa ataendelea kushinikiza kuhakikisha kuwa serikali ya Misri inayoongozwa na Rais Abdel Fattah al Sisi inachukuliwa hatua na Mahakama za Kimataifa kufuatia kifo cha Morsi. Wakati huo huo ameitaka Jumuiya ya OIC kuchukua hatua katika uwanja huo. Rais wa Uturuki amesema atawasilisha suala hilo katika mkutano wa G-20 uliopangwa kufanyika Japan baadaye mwezi huu.

Mohamed Morsi, Rais wa Misri aliyeaga dunia akiwa mahakamani

Mohamed Morsi alizikwa Jumanne asubuhi kimya kimya huko Cairo huku familia yake ikishuhudia muda mfupi baada ya kufariki dunia siku ya Jumatatu. Mazishi hayo yametajwa na wachambuzi wa mambo kuwa yanaibua shaka kuhusu namna kifo cha rais huyo wa zamani wa Misri kilivyotokea. 

Wakati huo huo Ofisi ya Kamisha Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa (OHCHR) juzi ilitoa taarifa ikitaka kufanyika uchunguzi huru na wa kina kuhusu kifo hicho.

Chanzo: parstoday.com

No comments:

Post a Comment