Mkuu wa Baraza la Kijeshi la Mpito la Sudan ameonana na Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini katika kikao cha faragha.
Abdul Fattah al Burhan jana Jumatatu alitembelea nchi jirani ya Sudan Kusini na kuonana na Rais Salva Kiir wa nchi hiyo ikiwa ni safari yake ya kwanza rasmi nje ya Sudan tangu aanze kuongoza baraza hilo la mpito la kijeshi.
Duru za kiserikali zimesema kuwa mazungumzo hayo yamefanyika faragha mbali na kamera za waandishi wa habari.
Wafuatiliaji wa mambo wamekisia kuwa kikao hicho kimehusiana na masuala ya utulivu wa kisiasa nchini Sudan na uhusiano wa nchi hizo mbili jirani.
Maandamano yanaendelea Sudan kulilazimisha Baraza la Kijeshi la Mpito likabidhi madaraka kwa raia
Baada ya jeshi la Sudan kufanya mapinduzi mwezi Aprili mwaka huu yaliyomng'oa madarakani Jenerali Omar al Bashir kutokana na maandamano makubwa ya wananchi, serikali ya Sudan Kusini ilikuwa ya kwanza kulitambua rasmi Baraza la Kijeshi la Mpito la Sudan.
Sudan imekumbwa na maandamano makubwa ya wananchi tangu tarehe 19 Disemba 2018 yaliyopelekea kuanguka utawala wa karibu miaka 30 wa Omar al Bashir. Hivi sasa maandamano hayo ya wananchi yanaendelea ili kulishinikiza Baraza la Kijeshi la Mpito la nchi hiyo kukabidhi madaraka kwa raia haraka iwezekanavyo.
Baraza hilo la mpito limehodhi madaraka ya Sudan tangu tarehe 11 Aprili mwaka huu na licha ya apatano na wapinzani lakini limekuwa likipoteza muda na kuchelewesha kutekeleza vipengee vya makubaliano ya pande mbili.
Chanzo: parstoday.com

No comments:
Post a Comment