Rais Nicolas Maduro wa Venezuela ameliamuru jeshi la nchi hiyo kujiweka tayari kukabiliana na hujuma tarajiwa ya Marekani. Aidha ametoa amri kwa makachero jeshini kuwasaka na kuwatia mbaroni askari wasaliti katika jeshi.
Katika ujumbe kupitia ukurasa wa Twitter Maduro amelitaka jeshi liwe tayari kulinda amani na kuzuia njama yoyote ya Marekani dhidi ya nchi hiyo.
Katika hotuba nyingine siku ya Jumanne mbele ya hadhara ya wanajeshi, Maduro aliliamuru jeshi kuwakamata askari wote wasaliti.
Amri hizo za Rais Maduro zimekuja baada ya Marekani kukariri mara kadha kuwa katika kukabiliana na Venezuela, 'machaguo yote' yako mezani.
Siku chache zilizopita, Jeshi la Venezuela lilitangaza utiifu kamili kwa serikali ya Rais Nicholas Maduro wa nchi hiyo na kusema liko na silaha mkononi tayari kukabiliana na hujuma yoyote ya kijeshi dhidi ya nchi hiyo.
Kinara wa upinzania Venezuela Juan Guaido (kulia) anayepata himaya ya utawala wa Rais Trump wa Marekani
Wanajeshi hao wamesema katu hawatairuhusu Marekani imefanikiwe katika hujuma dhidi ya nchi hiyo. Rais Maduro alitembea umbali wa maili moja akiwa pamoja na wanajeshi hao kabla ya kutoa hotuba kali ya kulaani ubeberu na ukoloni mamboleo wa Marekani.
Ikumbukwe kuwa, baada ya kushindwa katika uchaguzi wa rais, kinara wa upinzani Venezuela Juan Guaido alijitangaza kuwa rais wa muda hapo tarehe 23 Januari mwaka huu kupitia uungaji mkono kamili wa Marekani.
Hata hivyo licha ya njama hizo za kutaka kumuondoa madarakani Rais Maduro, jeshi na wananchi pamoja na nchi kama vile Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Russia, China, Afrika Kusini na mataifa mengi ya dunia yameendelea kusisitizia ulazima wa kuheshimiwa haki ya kujitawala nchi hiyo ya Amerika ya Latini.
Chanzo: parstoday.com

No comments:
Post a Comment