http://swahilivilla.blogspot.com/2014/01/mahojiano-na-faria-zam-kuhusu-msaada-wa.html

Thursday, May 30, 2019

Democrats waongeza shinikizo Trump avuliwe urais

Na Emmanuel Richard Makundi Imechapishwa 30-05-2019 Imehaririwa 30-05-2019 Saa 08:37

Saa chache baada ya aliyekuwa kiongozi wa timu ya wachunguzi kuhusu ikiwa Urusi iliingilia uchaguzi mkuu wa Marekani kufafanua kile kilichomo kwenye ripoti yake, wanasiasa watatu wa juu wa chama Democrats wametoa wito wa kuanzishwa mchakato wa kumuondoa madarakani rais Donald Trump.

media
Kiongozi wa lililokuwa jopo la uchunguzi, Robert Mueller.
REUTERS/Jim Bourg

Akizungumza kwa mara ya kwanza Jumatano ya wiki hii, Robert Mueller amesema uchunguzi walioufanya haukumfutia hatia rais Trump ya kukiuka sheria, akitofautiana pakubwa na matamshi ya Trump.

Mueller alikuwa amepewa jukumu la kuchunguza ikiwa Urusi iliingilia uchaguzi wa mwaka 2016.

Kwenye hotuba yake, Mueller amesema suala la kumfungulia mashtaka rais aliyeko madarakani halikuwa ni suala lililoko mezani kwa wakati ule.

Suala la mchakato wa kumuondoa Trump madarakani limewagawa wabunge wa chama cha Democrats, ambapo baadhi wamejitokeza kuongeza shinikizo kwa spika wa bunge Nancy Pelosi, ambaye mpaka sasa hajakubali kuanzisha mchakato huo.

Matamshi ya Mueller sasa yamewaibua wagombea wengine watatu wanaoomba kuchaguliwa na chama chao kuwania urais kwenye uchaguzi mkuu ujao, wakifanya idadi yao kuwa 10 ya wanaotaka mchakato wa kumuondoa Trump uanze.

Rais Trump kwa upande wake ameendelea kusisitiza kutokuwa na hatia akisema sheria zilizopo haziruhusu rais aliyeko madarakani kushtakiwa na hivyo mjadala wa Mueller umefungwa rasmi.

Chanzo: sw.rfi.fr

No comments:

Post a Comment