Baraza la Mpito la Kijeshi la Sudan limetangaza kuwa, limefikia makubaliano na wapinzani kuhusu kipindi cha miaka mitatu cha serikali ya mpito nchini humo.
Baraza hilo limetangaza kuwa, makubaliano kamili baina ya pande hizo mbili yatatangazwa katika kipindi cha masaa 24 yajayo.
Jenerali Yasir al Ata, mjumbe wa Baraza la Kijeshi la Sudan amesema kuwa, thuluthi mbili ya watu watakaounda serikali hiyo ya mpito watatoka katika Muungano wa Uhuru na Mageuzi na thuluthi moja iliyobakia watatoka katika vyama mbalimbali.
Mjumbe mmoja wa vyama vya upinzani nchini Sudan naye amesema kuwa, mitazamo ya pande hizo mbili yanakurubiana na karibuni hivi yatafikiwa makubaliano ya kutatua mgogoro wa nchi hiyo.
Maandamano ya wananchi wa Sudan yaliyomng'oa madarakani Omar al Bashir
Juzi Jumatatu kulifikiwa mapatano katika baadhi ya mambo baina ya Baraza la Kijeshi la Sudan na vyama vya upinzani pamoja na jumuiya ya kiraia inayojulikana kwa jina la Muungano wa Uhuru na Mageuzi.
Tangu tarehe 19 Disemba 2018 Sudan imekumbwa na malalamiko makubwa ya wananchi ambayo yamepelekea kung'olewa madarakani utawala wa takriban miaka 30 wa Omar Hassan al Bashir. Al Bashir hivi sasa anakabiliwa na tuhuma chungu nzima mahakamani zikiwemo za mauaji ya raia na kutakatisha fedha.
Tarehe 11 Aprili 2019 jeshi la Sudan lilitoa taarifa na kutangaza kupinduliwa Omar al Bashir na kuundwa Baraza la Mpito la Kijeshi, lakini wananchi wanaendelea na maandamano yao hadi hivi sasa wakilitaka baraza hilo la kijeshi likabidhi madaraka kwa raia haraka iwezekanavyo.
Chanzo: parstoday.com

No comments:
Post a Comment