Baraza la Mpito la Kijeshi la Sudan limekanusha taarifa kuwa limeafiki pendekezo lolote la kuundwa kwa Baraza huru la mpito.
Msemaji wa Baraza hilo Bw. Shams-Eddin Kabashi amesema, mpaka sasa, baraza hilo halijapokea waraka wowote kutoka timu ya upatanishi, na pia halijaongelea uwakilishi katika baraza huru. Pia amesema Baraza hilo linatarajia kukamilisha kusoma waraka uliowasilishwa na muungano wa upinzani, na kwamba litatoa majibu yake leo Jumatatu
Kamati ya upatanishi nchini Sudan inapandekeza kuundwa kamati ya watu 10 ya mpito itakayojumuisha raia saba na wanajeshi watatu chini ya uenyekiti wa Baraza la Kijeshi la nchi hiyo.
Licha ya kwamba jeshi la Sudan liliahidi kukabidhi madaraka kwa utawala wa kiraia baada ya maandamano kumng'oa madarakani rais wa zamani wa nchi hiyo, Omar Hassan al Bashir, lakini hadi sasa limeshindwa kutekeleza ahadi yake hiyo.
Maandamano Sudan
Baraza la Kijeshi la Sudan liliundwa baada ya mapinduzi ya kijeshi ya tarehe 11 mwezi uliopita wa Aprili, mapinduzi ambayo yalihitimisha utawala wa takriban miaka 30 wa Jenerali Omar Hassan al Bashir.
Baraza hilo lina wajumbe 9 wakiwemo wanajeshi sita, polisi wawili na afisa mmoja wa masuala ya kijasusi na usalama wa taifa.
Chanzo: parstoday.com

No comments:
Post a Comment