Rais Donald Trump wa Marekani jana Jumanne alitumia kura ya turufu kupinga mswada uliokuwa umepitishwa na Kongresi ya nchi hiyo kuhusu ulazima wa kukatwa misaada ya kijeshi ya Marekani kwa muungano wa kichokozi unaoongozwa na Saudi Arabia dhidi ya nchi masikini ya Yemen.
Mswada huo ulikuwa umepitishwa katika Seneti tarehe 14 mwezi Machi kwa kura 54 za ndio dhidi ya 46 za upinzani, ambapo uliwasilishwa kwenye Kongresi tarehe 4 Aprili na kupitishwa kwa kura 247 za ndio mkabala wa 175 zilizopinga.
Kabla ya hapo White House ilikuwa imetishia kwamba Trump angeupinga mswada huo kwa kura ya veto. Katika taarifa Trump aliutaja mswada huo kuwa hatari na uliolenga kupunguza nguvu zake.
Wabunge wa Kongresi walikuwa wamezidisha mashinikizo ya kutaka serikali ya Trump isimamishe ushirikiano wote wa kijeshi na utawala wa Saudi Arabia katika mashambulio yake huko Yemen, kufuatia mauaji ya kinyama ya Jamal Khashoggi, mwandishi mkosoaji wa utawala wa Riyadh na vilevile kufuatia kuvurugika hali ya kibinadamu huko Yemen kutokana na mashambulio ya muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudia dhidi ya watu wa nchi hiyo.
Kongresi imesimama dhidi ya Trump
Marekani imekuwa ikisaidia na kushirikiana kwa karibu kijeshi na Saudia katika mashambulio yake dhidi ya nchi hiyo na hivyo kuwa na mchango mkubwa katika kudumisha mgogoro wa nchi hiyo masikini ya Kiarabu. Saudia, Imarati na nchi nyingine kadhaa za Kiarabu zilianzisha mashambulizi ya kijeshi dhidi ya Yemen mwezi Machi 2015 na kuizingira kikamilifu nchi hiyo ardhini, baharini na angani.
Uvamizi wa nchi hizo dhidi ya Yemen kufikia sasa umepelekea Wayemen zaidi ya 15,000 kupoteza maisha, makumi ya maelfu ya wengine kujeruhiwa na mamilioni kuwa wakimbizi. Uchokozi huo wa kijeshi wa Saudia pia umepelekea Yemen kukabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula na dawa.
Chanzo: parstoday.com

No comments:
Post a Comment