Wizara ya Mambo ya Ndani ya Sudan imetangaza kuwa inaheshimu maandamano ya wananchi wanaotaka Rais Omar al-Bashir aondoke madarakani, na imewataka maafisa usalama kutowashambulia waandamanaji hao.
Hata hivyo wizara hiyo imetetea ukandamizaji wa hivi karibuni wa polisi na kudai kuwa maafisa hao wa usalama walikuwa wanatekeleza wajibu wao wa kikazi. Aidha imeongeza kwamba, baada ya kufuatilia matukio ya uvunjifu wa amani na jinai nchini Sudan wizara hiyo imeona ni vyema ikatoa maelekezo kwa makao makuu ya jeshi la polisi na kwa ofisi kuu za majimbo ya nchi hiyo kwamba maafisa hao wa kulinda usalama hawatakiwi kushambulia maandamano ya amani na badala yake watekeleze jukumu lao la kulinda usalama wa waandamanaji hao.
Sehemu ya maandmano nchini Sudan
Amri hiyo imekuja kufuatia matukio ya hivi karibuni yaliyoshuhudiwa Khartoum, mji mkuu wa Sudan wakati polisi walipotaka kuwakandamiza waandamanaji mbele ya Wizara ya Ulinzi, na kupelekea kuzuka ghasia kubwa na watu wengi kujeruhiwa.
Aidha Wizara ya Mambo ya Ndani ya Sudan imewasihi wananchi kufanya maandamano ya amani na kujiepusha na vitendo vya uharibifu. Kadhalika imesisitizia haja ya kufanyika mabadiliko ya uongozi kwa njia za amani.
Hii ni katika hali ambayo nchi kadhaa kama vile Uingereza, Marekani na Norway zimetoa taarifa ya pamoja zikiitaka serikali ya Sudan kutekeleza matakwa ya waandamanaji wanaotaka mabadiliko ya kisiasa nchini humo.
Chanzo: parstoday.com

No comments:
Post a Comment