Chama cha Umma chasema al Bashir lazima ang'oke madarakani nchini Sudan
Upinzani dhidi ya Rais Omar al Bashir wa Sudan unaendelea kila upande huku waandamanaji wakizidi kung'ang'ania msimamo wao wa kumtaka ang'oke madarakani. Katika tukio la karibuni kabisa chama cha upinzani cha Umma kwa mara nyingine kimesema kuwa al Bashir lazima aachie madaraka.
Televisheni ya al Hadath imemnukuu Ibrahim al Amin, Naibu Mwenyekiti wa chama cha Umma cha Sudan akisema kuwa, serikali ya Rais Omar al Bashir ndiyo sababu kuu ya mgogoro wa hivi sasa wa nchi hiyo.
Chama hicho cha upinzani kimesema katika taarifa yake rasmi kwamba serikali iliyoko madarakani hivi sasa huko Sudan lazima ijiuzulu na taasisi zake zote ili kutoa fursa ya kuundwa serikali ya mpito.
Rais Omar al Bashir wa Sudan
Wananchi wa Sudan jana waliendelea kuandamana kwa maelfu mjini Khartoum mbele ya jengo la wizara ya ulinzi ya nchi hiyo huku jeshi la nchi hiyo nalo likiwahami waandamanaji hao mbele ya polisi na vikosi vya usalama vya serikali ya Rais al Bashir.
Maandamano ya wananchi wa Sudan ni makubwa kiasi kwamba hayajawahi kushuhudiwa mfano wake katika kipindi cha miaka 30 iliyopita. Maandamano ya hivi sasa yalianza mwezi Disemba 2018 kulalamikia kupanda kwa bei za bidhaa muhimu hasa mkate na mafuta.
Waandamanaji wanamtuhumu Rais Omar al Bashir na serikali yake kuwa wamevuruga uchumi wa nchi hiyo na wanamtaka yeye na taasisi zote za serikali zing'oke madarakani.
Chanzo: parstoday.com/
No comments:
Post a Comment